Saturday, November 5, 2016

Prof.Ndalichako awahakikishia mkopo wanachuo wanaoendelea

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amewahakikishia wanafunzi wanaoendelea na masomo wakinufaika na mkopo kupitia Bodi ya Mkopo wa Elimu ya Juu kuwa hakuna atakayefutiwa mkopo. Profesa Ndalichako aliyasema hayo jana Bungeni mjini Dodoma katika kikao cha Bunge la 11 kinachoendelea. “Serikali haijafuta mkopo kwa mwanafunzi yoyote ambaye anaendelea na masomo yake,” alisema Profesa Ndalichako na kuongeza kuwa kuchelewa kwa mkopo kumetokana na vyuo husika kuchelewa kuwasilisha matokeo ya wanafunzi wanaoendelea kwani hutumika kuwatambua wanafunzi wanaokidhi kigezo cha ufaulu.

Rais Magufuli atoa majibu

Rais Magufuli ajibu madai ya kukandamiza demokrasia na Udikteta


Rais John Magufuli ameyatolea majibu malalamiko yaliyokuwa yakitolewa na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani nchini kuwa amekuwa akikandamiza demokrasia tangu alipoingia madarakani.

Akijibu swali lililoulizwa na mmoja kati ya wahariri wa vyombo vya habari leo Ikulu jijini Dar es Salaam, aliyetaka ufafanuzi kuhusu malalamiko hayo, Rais Magufuli alisema kuwa hajawahi kukandamiza demokrasia nchini na kwamba anachofanya ni kuihuisha.

“Katika kazi yoyote, critic ni kitu cha kawaida na pongezi ni kitu cha kawaida. Lakini ukweli ni kwamba katika muda wote ambao nimechaguliwa kuwa Rais sija-suppress democracy (sijakandamiza demokrasia) na bahati nzuri ninapromote demokrasia,” alisema Rais Magufuli.

“Na ndio maana unaona Bunge linaendelea vizuri. Na ndio maana unaona uchaguzi unafanyika hata hapa Dar es Salaam kuna maeneo wamechagua Ukawa na kuna maeneo wamechagua CCM. Hiyo ni demokrasia. Mikutano yao ya ndani ya vyama mmekuwa mkishuhudia, na hivi juzijuzi kumekuwa na mkutano wa chama fulani, wakagombana wenyewe na wakafukuzana wenyewe,” aliongeza.

Aidha, akijibu swali la nyongeza lililoulizwa na mwanahabari mkongwe, Tido Mhando (Azam TV) kuhusu mtazamo wa baadhi ya watu kuwa huenda anaendesha mambo kidikteta bila kufuata taratibu zilizowekwa, Rais Magufuli alisema hiyo ni tafsiri ya mtu ambayo inatokana na uhuru wa kufikiria.

“Kila mmoja anaweza akatafsiri vyovyote… wewe(Tido) ulipokuwa BBC ukahama ukaenda TBC, ukahama leo uko Azam, mtu mwingine anaweza akatafsiri kuwa huenda huo ni udikteta wa namna fulani wa kuhamishwahamishwa. Kwa hiyo kila mmoja ana uhuru wa kufikiria anavyofikiria,” alisema.

Rais Magufuli leo amefanya mkutano na Wahariri wa vyombo vya habari kwa lengo la kujibu maswali yao

Bodi ya Mikopo Elimu Ya Elimu ya Juu Yaagizwa

Bodi ya Mikopo Ya Elimu ya Juu Yaagizwa Kuwapa Wanafunzi Fedha Zao ifikapo Leo

Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELSB), imeagizwa kuhakikisha kuwa fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wanaoendelea na masomo zinapelekwa vyuoni ifikapo leo. 

Agizo hilo lilitolewa bungeni jana na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako baada ya wabunge mbalimbali kuomba miongozo kwa Spika kuhusu kuwapo kwa wanafunzi wengi waliokosa mikopo kwa mwaka wa fedha 2016/17. 

Mwongozo kwa Spika ulitiliwa mkazo na Mbunge wa Chalinze (CCM), Ridhiwan Kikwete aliyeeleza kuwapo taarifa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kuwa wanafunzi wanataka kugoma kwa kukosa fedha za mikopo. 

Kutokana na miongozo hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga aliitaka Serikali kutoa maelezo. 

Akitoa kauli ya Serikali, Profesa Ndalichako alisema fedha za mikopo kwa ajili ya wanafunzi zilikwenda vyuoni wiki moja iliyopita. 

“Tatizo lililotokea kwa UDSM sijui kama walidanganyana au la lakini hawakujaza fomu. Serikali haitatoa mkopo kwa mwanafunzi ambaye hajajaza fomu. Na waliosaini leo wataingiziwa fedha zao kwenye akaunti na vyuo,”alisema. 

Kuhusu wanaoendelea na masomo, Profesa Ndalichako alisema wanafunzi wote wanufaika na wanaoendelea na masomo wataendelea kupatiwa mikopo kama ilivyokuwa mwaka uliopita. 

Alisema wanafunzi ambao vyuo vyao vimewasilisha HELSB taarifa za matokeo, Bodi imekwishawatumia fedha vyuoni kwa ajili ya kuwapa mikopo wanafunzi hao. 

Hata hivyo, alisema taratibu za kuwabaini wanafunzi wenye sifa zinaendelea na wasio na sifa wataendelea kuondolewa kupata mikopo. 

Pia, alikiri kuwa ucheleweshaji wa matokeo ya wanafunzi wanaoendelea na masomo umeathiri kasi ya kutuma fedha vyuoni. 

“Wizara yangu imekwishaagiza vyuo vyote ambavyo havijawasilisha matokeo ya mitihani ya wanafunzi wao kwa mwaka wa masomo uliopita, kufanya hivyo mara moja,”alisema. 

Ndalichako alisema hadi kufikia Novemba 3 mwaka huu, Sh71.042 bilioni zilikwishatumwa vyuoni kwa ajili ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wanaoendelea na masomo.

Akizungumzia utoaji wa mikopo kwa mwaka wa fedha 2016/17, Ndalichako alisema katika mwaka huo, Sh483 bilioni zimetengwa na zimelenga kutoa mikopo kwa wanafunzi 119,012, wanafunzi 93,295 wanaoendelea na masomo na wa mwaka wa kwanza 25,717.

Ndalichako alisema katika mwaka wa fedha 2016/17 wanafunzi 58,010 walidahiliwa na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na orodha yao iliwasilishwa HELSB na hadi Novemba 2, mwaka huu, wanafunzi 21,190 wa mwaka wa kwanza wamepewa fedha. Kati yao 4,321 ni yatima, 118 wenye ulemavu na 87 ni waliosoma sekondari kwa ufadhili wa taasisi mbalimbali.