Sunday, November 20, 2016

Lowassa alionewa CCM

Bashe adai Lowassa alionewa CCM, aeleza uhusiano wao kwa sasa


Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe (CCM) amesema kuwa anaamini waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliondolewa kwa kuonewa katika mchakato wa kugombea urais ndani ya CCM.

Bashe amesema kuwa kitendo hicho alichokiita cha kiuonevu ni changamoto kubwa ndani ya CCM na kwamba wengi wameonewa katika michakato ya kuwania nafasi mbalimbali.

“Yaliyomkuta Lowassa yamewakuta wengi ndani ya CCM, hivyo jambo hilo sio geni,” Bashe anakaririwa na Mwananchi. “Wapo waliobaki na wapo walioamua kuhama chama kwa sababu ni binadamu. CCM ina historia hiyo, hii ndiyo changamoto yake kubwa,” aliongeza.

Mbunge huyo alifafanua kuwa kwakuwa Lowassa alituhumiwa kwa mengi ndani ya chama hicho, alipaswa kuitwa na kuelezwa tuhuma zake na sababu za kuondolewa jina lake ili umma ufahamu.

Alisema kuwa katika chama hicho, kashfa nyingi hufanywa kwa sababu maalum na hubuniwa kwa ajili ya kufikia lengo fulani dhidi ya mtu au kikundi cha watu.

Alisema kuwa mbali na sakata la Richmond lililopelekea Lowassa kujiuzulu nafasi ya uwaziri mkuu, masakata ya Lugumi na Tegeta Escrow ni sehemu yale yaliyobuniwa kwa lengo maalum.

“Tazama wanavyofunika sakata la Lugumi. Usiende mbali angalia sakata la Escrow. Tumeadhibu waliopata fedha kutoka benki ya Mkombozi, vipi wa Stanbic? Wizi mwingine uliofanywa nchi hii una uhusiano kati ya Serikali na vikundi vya watu wenye uhusiano na Serikali,” Bashe aliliambia Mwananchi.

Akizungumzia uhusiano wake na Lowassa ambaye alikuwa anamuunga mkono wakati wa mchakato wa kugombea urais kupitia CCM, Bashe alisema hivi sasa hawana uhusiano tena wa urafiki wa kisiasa.

Alisema kuwa alimshauri sana Lowassa kutohama CCM, avumilie, lakini hakufanikiwa kumshawishi, hivyo waliagana.

“Lowassa ni mzee wangu. Ni mtu ambaye namheshimu na nitaendelea kufanya hivyo, ingawa kwa sasa hatuna uhusiano wa kisiasa,” alisema.

Lowassa alihama CCM baada ya jina lake kukatwa katika mchakato wa kuwania urais, alihamia Chadema na kupewa nafasi ya kugombea urais katika uchaguzi unaotajwa kuwa na ushindani mkali zaidi tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi.

Akataa Kulipwa Mshahara wa Urais

Donald Trump Akataa Kulipwa Mshahara wa Urais

Rais mteule wa Marekani, bilionea Donald Trump amesema hatakubali kupokea mshahara wa urais pindi atakapokuwa madarakani.

Trump ameweka msimamo huo jana katika mahojiano maalum na mtangazaji maarufu, Lesley Stahl katika kipindi cha 60 Minutes, aliyetaka kufahamu kuhusu uamuzi wake juu ya mshahara wake akiwa ni mfanyabiashara mkubwa.

“Sijawahi kuzungumzia hili, lakini jibu langu ni hapana,” alisema. “Nafikiri inanibidi kupokea kwa mujibu wa sheria $1, kwahiyo ntachukua $1 (Sawa na shilingi 2,200 za Tanzania) kwa mwaka. Lakini hata sijui ni nini,” aliongeza.

Ingawa mtangazaji huyo alimkumbusha Trump kuwa anaiacha $400,000 kwa mwaka, rais huyo mteule alisisitiza, “sitachukua mshahara. Sitapokea.”

Wakati wa kampeni, Trump aliahidi kuwa atajiweka kando na biashara zake endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Marekani, na kwamba atajikita zaidi katika kutimiza ahadi zake kwa Wamarekani. Alisema kuwa biashara zake ataziacha mikononi mwa watoto wake.

Wasira Kukata Rufaa tena

Wapambe wa Wasira Kukata Rufaa tena Kupinga Ushindi wa Bulaya

Baada ya Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza kutupilia mbali maombi ya wananchi wanne wa kutaka itengue ushindi wa Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini Ester Bulaya (Chadema), walalamikaji hao wamesema watakata rufaa katika Mahakama ya Rufaa kwa kile walichosema kuwa Mahakama hiyo haikutenda haki katika kutoa maamuzi hayo.

Novemba 18, mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza iliyokuwa inasikiliza kesi hiyo namba moja ya mwaka huu, katika Mahakama ya Mkoa wa Mara mjini Musoma, chini ya Jaji Noel Chocha, ilitupilia mbali kesi hiyo na kumthibitisha Bulaya kuwa ni Mbunge halali wa jimbo hilo.

Wananchi hao wanne walikuwa wamefungua kesi hiyo wakipinga ushindi wa Bulaya dhidi ya Stephen Wasira kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana.

Baada ya hukumu hiyo kutolewa waandishi wa habari walimhoji mmoja wa walalamikaji Janes Ezekiel, ambaye alisema kuwa watakaa na wenzake waone namna ya kukata rufaa.

Hata hivyo baadaye mlalamikaji mwingine Ascetic Malagila alimwambia mwandishi wa habari hii kuwa tayari wamekubaliana na wenzake pamoja na mwanasheria wao kuwa watakata rufaa katika Mahakama ya Rufaa kupinga hukumu hiyo, kwa kile alichoeleza kuwa wameshindwa kwa sababu ya uonevu na kwamba watatafuta haki yao katika Mahakama ya Rufaa.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Wasira alidai kuwa tayari walalamikaji hao pamoja na wakili wao Constantine Mutalemwa, wamekutana na kukubaliana kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa kutafuta haki.

Kabla ya hukumu hiyo kutolewa Jaji Chocha, alirejea baadhi ya vifungu vya sheria pamoja na hoja mbalimbali zilizotolewa na waleta maombi (walalamikaji) na wajibu maombi wa kwanza, wa pili na watatu.

Jaji Chocha alisema kuwa kutokana na kupitia vifungu vyote vya sheria pamoja na ushahidi uliotolewa na waleta maombi katika Mahakama hiyo, ni kwamba ushahidi wao haujajitosheleza katika hatua ya kutengua ubunge wa jimbo hilo.

Alisema kuwa iwapo ataamua kufuta matokeo hayo atawasababishia wananchi wa jimbo hilo ambalo ni miongoni mwa jimbo lenye watu masikini sana kukosa haki yao.

Alisema kuwa madhara ya kurudia uchaguzi ni makubwa sana, sanjari na gharama za uendeshaji wa uchaguzi mpya, ambao utaligharimu taifa na wananchi kwa ujumla kwa sababu gharama za uchaguzi ni sehemu ya kodi ya kila mwananchi.

Akirejea mwenendo mzima wa kesi hiyo tangu ilipofunguliwa katika Mahakama hiyo, Jaji huyo alikiri kutokea kwa kasoro kadhaa katika kipindi cha uchaguzi hadi kutangaza matokeo na kusema kuwa ni kawaida ya uchaguzi wowote kuwa na kasoro ndogondogo na kuongeza kuwa hata nchi zilizoendelea kasoro huwa hazikosekani.

Alisema kuwa katika kesi hiyo kasoro nyingi zilizojitokeza zimeonekana mara baada ya matokeo kutangazwa, lakini katika mchakato mzima wa upigaji kura hakuna kasoro zilizobainishwa, ambazo zingeweza kuonekana kwenye fomu yoyote ya malalamiko anayokuwa nayo msimamizi wa uchaguzi, ambazo zingeonesha kuwa uchaguzi haukuwa wa huru na haki. Alibainisha kuwa si kila kasoro inayojitokeza kwenye uchaguzi inaweza kuathiri matokeo ya uchaguzi.

Hata hivyo alisema kuwa pia msimamizi wa uchaguzi huo Lucy Msoffe alifanya uzembe mkubwa sana wakati alipofika katika hatua ya kuandika idadi ya wapiga kura na kwamba alipaswa kuwa makini kwa kutokuandika takwimu kimakosa.

Akizungumza nje ya Mahakama hiyo wakili wa mjibu maombi Paul Kipeja, alisema maamuzi yaliyotolewa na Mahakama hiyo waliyatarajia tangu mwanzo wa kesi hiyo kwa sababu hakukuwa na hoja zozote za msingi za waleta maombi.

Kuhusu gharama walizotumia katika kesi hiyo wakili Kipeja alisema kuwa watakaa pamoja na wakili Tundu Lissu, ili waweze kurudishiwa gharama zao zote walizotumia kuendeshea kesi hiyo.