Monday, November 7, 2016

Tanesco yaomba kupandisha bei ya umeme



MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imepokea maombi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ya kupandisha gharama za umeme kwa asilimia 18.19 kuanzia mwaka ujao.

Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imeeleza kuwa Oktoba 4, mamlaka hiyo ilipokea ombi la mabadiliko ya bei ya umeme, hivyo unaandaliwa mkakati wa kukusanya maoni ya wadau wa nishati hiyo.

“Mikutano ya ukusanyaji maoni kuhusu bei inayopendekezwa na Tanesco itaanza Novemba 16 katika mikoa ya Mwanza, Mbeya, Arusha, Dodoma  na kwa Dar es Salaam ni Novemba 23,” inaeleza taarifa hiyo.

Aprili mwaka huu, Tanesco ilituma maombi kwa Ewura ya kupunguza gharama za umeme kwa asilimia 1.1, lakini baada ya mamlaka hiyo kupitia maombi hayo, ilipunguza gharama hizo kwa asilimia 1.5 hadi 2.4.

Bei ya sasa baada ya punguzo hilo la Ewura kwa wateja wa shirika hilo, kutoka kundi la D1 wanaotumia kiasi cha umeme kuanzia kilowati 0 hadi 75 ni Sh 100 na zaidi ya kilowati 75 kwa mwezi wanatozwa Sh 350 kwa uniti moja.

Aidha, kwa wateja wa kundi la T1 ambao ni kuanzia majumbani, viwandani na biashara ndogo ndogo hutozwa kiasi cha Sh 292 kwa uniti moja na kwa wateja wa kundi T2 ambalo ni kundi linalotumia umeme kuanzia kilowati 7,500 hutozwa kwa wastani wa Sh 15,004 kwa mwezi kwa uniti moja.

Kwa makundi ya T3 na T4 wanaotumia umeme mkubwa kama vile kwenye machimbo, viwanda vikubwa na Mamlaka ya Umeme Zanzibar (ZECO) yenyewe hutozwa kiasi cha Sh 13,200 hadi 16,550 kwa mwezi kwa uniti moja.

Hata hivyo, kutokana na ombi hilo la ongezeko la bei kwa asilimia 18.19, sasa wateja wa kawaida wanaotumia umeme kuanzia kilowati hadi 75 watakuwa na ongezeko la Sh 18 ambapo endapo ombi hilo likiridhiwa watatozwa Sh 118 kwa uniti moja.

Aidha, kwa wateja wanaonunua umeme zaidi ya kilowati 75 ambao kwa sasa wanatozwa Sh 350 kwa uniti moja, endapo ombi hilo likipitishwa watakuwa na ongezeko la bei la Sh 63 hivyo watatozwa kiasi cha Sh 413 kwa uniti moja.

Kwa upande wa wateja wa kundi la T1 ambao ni kuanzia majumbani, viwandani na biashara ndogo ndogo wanaotozwa kwa sasa kiasi cha Sh 292, watakuwa na ongezeko la Sh 52.56 hivyo endapo ombi hilo litaridhiwa bei hiyo itapanda na kufikia Sh 344.56 kwa uniti moja.

Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo pamoja na kuthibitisha mamlaka hiyo kupokea maombi hayo, alisisitiza kuwa bado ombi hilo linachambuliwa na kufanyiwa tathmini na mamlaka hiyo kabla ya kuidhinishwa.

Waliokula Fedha za Mikopo Elimu ya Juu Kitanzini....


Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali Namba 3 wa Mwaka 2016 unatarajiwa kuwasilishwa bungeni leo, ukigusa sheria tisa ikiwemo ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu ambapo sasa mnufaika wa mkopo aliyejiajiri atalipa kiasi kisichopungua Sh 120,000 au asilimia 15 ya kipato chake, huku taasisi za umma, bodi, wakala na tume zimebanwa zisirekebishe au kuwianisha mishahara, posho na marupurupu kwa watumishi.

Kwa mujibu wa muswada huo, kwenye Sheria ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu, waajiri wanaoshindwa kuwasilisha marejesho ya mwezi baada ya makato wataadhibiwa, ambapo mwajiri atawajibika kuitaarifu Bodi ya Mikopo kuhusu ajira ya mtu yeyote ambaye ana shahada au stashahada na kukata makato ya mwezi kutoka kwenye mshahara wa mnufaika wa mkopo.

Kifungu hicho kinapendekeza kufanya marejesho ya mkopo kuwa ya kisheria na kupewa nafasi ya awali katika orodha ya makato na kinapendekeza kupunguzwa idadi ya wajumbe wa Bodi ya Mikopo na kufikia saba kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji.

Kwenye marekebisho ya Sheria ya Utumishi wa Umma, Kifungu cha 8 kinapendekeza kufanyiwa marekebisho ili kumpa mamlaka Katibu Mkuu (Utumishi) kurekebisha na kuwianisha mishahara, posho na marupurupu mengine kwa watumishi wa umma.

Inapendekezwa kumuondolea Katibu mamlaka ya kuteua watumishi wa umma wanaounda baraza la majadiliano ya pamoja ya watumishi wa umma na sasa waziri atateua katibu kutoka wizara yenye dhamana na kada husika ya watumishi.

Pia inapendekezwa kufuta kifungu cha 11 ili kuondoa masharti yanayokataza Baraza la majadiliano ya pamoja ya watumishi na baraza la pamoja la watumishi wa umma kutoa mapendekezo kuhusu ujira.

Kwa upande wa marekebisho ya Sheria ya Leseni na Usafirishaji, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kutaongezwa kifungu ili kuweka masharti yanayoruhusu ulipwaji wa faini pale mkosaji anapokiri kosa, badala ya kila kosa kufuata taratibu za kimahakama.

Muswada huo una marekebisho kwenye Sheria ya Mazingira ambako kutawekwa mwongozo wa namna ya kupima urefu wa mita 60 kwenye kingo za bahari, ziwa, mto au bwawa la maji kinachozuiliwa kufanyia shughuli zozote za binadamu. Upimaji utapimwa kuanzia kwenye kingo za maeneo hayo.

Sheria nyingine zitakazofanyiwa marekebisho kwenye Mkutano wa Tano wa Bunge la 11 ni ya Usafiri wa Anga, Sheria ya Msajili wa Hazina na Sheria ya Vipimo.

Spika Job Ndugai wakati akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Tano wa Bunge wiki iliyopita, alieleza kuwa kwa wiki hii Bunge litapokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali(CAG) ya mwaka 2014/2015 kisha kujadili na kuishauri serikali kuhusu Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Jumuiya ya Ulaya (EU) na Afrika Mashariki (EPA-EU) na kisha taarifa ya kamati ndogo kuhusu uchambuzi wa sheria ndogo

Samweli Sitta afariki dunia


Spika wa Bunge Mstaafu, Samuel Sitta (74) amefariki dunia usiku wa kuamkia leo wakati akipatiwa matibabu nchini Ujerumani.

Mtoto wa marehemu, Benjamin Sitta amesema baba yake amefariki saa 10:00 usiku wa kuamkia leo.

‘’Nikweli mzee amefariki nchini Ujerumani akiwa anapatiwa matibabu, alipelekwa Alhamisi iliyopita na alikuwa anasumbulia na saratani ya tezi dume ambayo ilisambaa na kuathiri miguu na mwili mzima."

Benjamin amesema kuwa taarifa za mipango ya kusafirisha mwili zitatolewa baadaye.

Sitta alikuwa Spika wa Bunge tangu mwaka 2005 hadi mwaka 2010 na pia mbunge wa Urambo Mashariki.

Pia, alikuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba na aliwahi kuwa waziri katika wizara mbalimbali kwa vipindi tofauti.

Alikuwa miongoni mwa wanachama zaidi ya 42 wa CCM waliochukua fomu za kugombea urais mwaka jana.