Thursday, November 3, 2016

Taarifa Kwa Umma Kutoka Jeshi La Polisi Makao Makuu.


Jeshi la Polisi nchini, katika kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unaimarika, limeendelea na operesheni za kukamata wahalifu wa makosa mbalimbali yakiwemo makosa ya usalama barabarani katika mikoa yote ili kudhibiti vitendo vya uhalifu na wahalifu. 

Katika operesheni hizo, Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata silaha na katika baadhi ya mikoa, wananchi wameweza kusalimisha silaha kwa hiari katika vituo vya Polisi.

Operesheni hizi ni endelevu, na ili tuweze kufanikiwa zaidi katika kudhibiti uhalifu na wahalifu hususani katika kipindi hiki tunapoelekea mwisho wa mwaka, wananchi wanatakiwa kuwa makini na kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu haraka kwa kutumia namba za bure 111 na 112 pindi wanapowatilia shaka watu wasiowajua katika maeneo yao ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.

Kwa wamiliki wa maduka makubwa, hoteli na maduka ya kufanyia miamala ya fedha kwa njia ya simu waangalie namna ya kuweka vifaa maalumu vyenye uwezo wa kurekodi mienendo ya watu wanaoingia na kutoka ama kufuata huduma katika maeneo yao ya biashara.

Pia, wananchi katika makazi yao waimarishe ulinzi kwa kutumia mpango wa ulinzi jirani kwa kuhakikisha wanakuwa na utaratibu wa kubadilishana taarifa za hali ya usalama ili kuhakikisha mitaa yao inakuwa salama wakati wote.

Aidha, Jeshi la Polisi nchini linawataka madereva wa vyombo vya moto kuheshimu na kutii sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali na kuokoa maisha ya abiria na watumiaji wengine wa barabara. 

Jeshi la polisi nchini, litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria, bila woga ama upendeleo katika kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unaimarika.

Imetolewa na:
Advera John Bulimba - Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP)
Msemaji wa Jeshi la Polisi,
Makao Makuu ya Polisi.

Rais Magufuli Aishauri Benki ya Dunia

Rais Magufuli Aishauri Benki ya Dunia kutoa Mikopo kwa wakati unaofaa ili utekelezaji wa miradi ufanyike kwa haraka.

SeeBait
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 03 Novemba, 2016 amekutana na Mwakilishi wa Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia Bi. Bella Bird na kuzungumzia utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini Tanzania yenye thamani ya jumla ya Dola za Marekani Bilioni 1.6 zikiwa ni mkopo kutoka benki hiyo.

Akizungumza baada ya kumaliza mazungumzo yake na Rais Magufuli, Bi. Bella Bird amesema mikopo hiyo inalenga kusaidia juhudi za maendeleo nchini Tanzania na itatolewa katika sekta mbalimbali zikiwemo nishati, usafirishaji, elimu na maji.

"Miradi hii yote imelenga zaidi kuharakisha maendeleo na kuleta matokeo katika maisha ya Watanzania, ni miradi ambayo inahitaji uongozi na msukumo mzuri kutoka Serikalini na tunafurahi kwamba Rais Magufuli ni kiongozi ambaye ana dhamira ya dhati ya kusimamia maendeleo" amesema Bi. Bella Bird.

Kwa upande wake Rais Magufuli ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika maendeleo na ametoa wito kwa Benki hiyo kuharakisha utoaji wa mikopo kwa ajili ya kutekeleza miradi.

"Tunataka kuona mambo yanatokea badala ya kutumia muda mwingi kuzungumza, miradi hii ina manufaa makubwa kwa watanzania na tungependa utekelezaji wake ufanyike haraka, na ili ufanyike haraka Benki ya Dunia inapaswa kutupatia mikopo kwa wakati unaofaa"amesisitiza Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli amemhakikishia Bi. Bella Bird kuwa Serikali yake ya Awamu ya Tano imejipanga kusimamia utekelezaji wa miradi yote inayotekelezwa sasa na itakayoanza kutekelezwa katika siku zijazo kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia.

Kwa hivi sasa miradi 26 yenye thamani ya Jumla ya Dola za Marekani Bilioni 4.5 inatekelezwa hapa nchini kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

SERIKALI YAVIAGIZA VYUO VIKUU NCHINI

Serikali kupitia Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Maimuna Tarish imevitaka vyuo vikuu 14 ambavyo havijatuma matokeo ya wanafunzi wao ya mwaka uliopita kwa Bodi ya Mikopo kutuma mara moja ili kuwapatia mikopo kwa walio katika utaratibu wa kupata mkopo wa serikali.

Taarifa ambayo imetolewa na Tarish imevipa vyuo hivyo 14 siku mbili pekee kuhakikisha vinatuma majina kwa Bodi ya Mikopo na kuagiza viweke mfumo mzuri ambao utawawezesha kutuma matokeo kwa haraka.

HUJUMA BODI YA MIKOPO (HESLB)

Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu nchini limemuomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa hesabu za Sh bilioni 1.74 za ada ya uombaji mikopo kwa mwaka huu katika Bodi ya Mikopo (HESLB) ili kujua matumizi ya fedha hizo kwa kuwa kuna mapungufu.

Aidha, shirikisho hilo limedai kubaini hujuma katika bodi hiyo zinazofanywa kwa makusudi ili kuchafua utendaji wa serikali iliyopo madarakani.

Hayo yalisemwa jana na Katibu Mtendaji wa shirikisho hilo, Daniel Zenda alipokuwa anazungumzia tuhuma za hujuma hizo, akidai zinafanywa kwa makusudi ili kurudisha nyuma jitihada njema za serikali.

Alisema ofisi ya CAG inapaswa kufanya ukaguzi wa Sh bilioni 1.74 fedha ambazo zilitokana na ada ya uombaji wa mikopo kwa mwaka huu ambapo kila mwanafunzi alitoa Sh 30,000 kwa waombaji 54,000.

Alisema ni muhimu kujua matumizi ya fedha hizo kutokana na upungufu uliojitokeza katika upitiaji wa sifa na vigezo vya wanaostahili kupata mkopo.

Alifafanua kuwa wanatambua hatua ya serikali katika kuhakikisha wanafunzi wenye sifa wanapata mikopo kwa wakati ambapo takribani Sh bilioni 80 zimeongezwa kwenye bajeti ya bodi hiyo ili kuwezesha mikopo kwa wanafunzi wote wenye sifa.

Zenda alisema Sh bilioni 487 zimepitishwa katika bajeti ya mwaka huu na mwaka jana ilikuwa chini ya makadirio ya Sh bilioni 350, lakini pamoja na kuongezeka kwa fedha hizo idadi ya wanafunzi walionufaika na mikopo imekuwa pungufu.

“Mwaka uliopita wanufaika wa mikopo walikuwa 53,000 na mwaka huu wanufaika wanafunzi 25,700 pamoja na ongezeko la makadirio ya zaidi ya Sh bilioni 137 kwenye bajeti ya Mikopo bado wanafunzi wengi hawajafikiwa,” alisema.

KUVUJA KWA MITIHANI YA KIDATO CHA NNE

Walimu wa Shule ya Sekondari Hasanga, iliyopo wilayani Mbozi mkoani Songwe na wafanyabiashara wawili, wanahojiwa na vyombo vya usalama mkoani Mbeya kwa tuhuma za kuhusika na utengenezaji wa mitihani feki ya kidato cha nne.

Watuhumiwa hao, James Kapinga (36) ambaye anadaiwa kufanya kazi Shule ya Sekondari ya Hasanga pia anajitolea kufundisha Shule ya Sekondari ya Wazazi ya Sangu, Baraka Mwazambe (28), mfanyabiashara na mkazi wa Tunduma na mtaalamu wa masuala ya Tehama (IT), Alex Mochi.

Watu hao kwa pamoja inadaiwa walikamatwa juzi usiku baada ya mwanafunzi mmoja ambaye jina lake na la shule vimehifadhiwa kukutwa na mtihani wa somo la Kiingereza na alipobanwa, inadaiwa aliwataja wahusika hao.

“Mwanafunzi huyu ni wa shule nyingine tena si ya Mbeya, alikutwa na mtihani feki wa somo la Kiingereza, alipohojiwa alieleza mtihani huo ulitoka Mbeya na Serikali ilipofuatilia iliwabaini wahusika ambao walikuwa wanasambaza mitihani feki,” kilisema chanzo kimoja cha habari hii.

Akizungumzia sakata hilo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Mariamu Mtunguja, alikiri ofisi yake kupokea taarifa juu ya uvujaji wa mitihani na walipofuatilia walibaini mitihani hiyo ni feki.

“Mbeya hakuna mitihani iliyovuja kama inavyoelezwa katika mitandao, ukweli ni kwamba suala hilo lilifuatiliwa ilibainika mitihani inayosambazwa si ile iliyochapishwa na Baraza la Mitihani la Taifa, ni feki na baadhi ya wahusika wanahojiwa na vyombo vya dola,” alisema.

Naye Kaimu Ofisa Elimu Mkoa wa Mbeya, Benedict Sandy, alisema hakuna mitihani iliyovuja.

“Mitandao imekuwa ikitoa taarifa za upotoshaji eti mitihani imevuja, mitihani iliyosambaa na kukutwa na baadhi ya wanafunzi tena si wa Mkoa wa Mbeya ni feki na wahusika wanaodaiwa kuisambaza wamekamatwa.

“Nawaomba wanafunzi wazingatie yale waliyofundishwa, mitihani hiyo inakuja kwa lengo baya la kuwapotezea muda wao na mwisho wa siku kuishia kufeli, watu wanaofanya kazi hiyo wapo kimasilahi,” alisema.

KESI YA SCORPION

Upande wa Jamhuri kwenye kesi ya Salim Njwete  maarufu kama 'Scorpion' anayetuhumiwa kumwibia Saidi Mrisho na kumtoboa macho kwa kisu umedai mahakamani hapo kwamba upelelezi haujakamilika na kuomba siku nyingine ya kukamilisha.

Mshitakiwa Njwete 34,  anashitakiwa kwa kumwibia Mrisho na kumjeruhi kwa kumchoma tumboni, mabegani na machoni.

Taarifa ya upelelezi kutokamilika ilielezwa jana na Mwendesha Mashitaka Chensensi Gavyole mbele ya Hakimu Mkazi Flora Haule kesi hiyo ilipotajwa na kuangaliwa kama upelelezi umekamilika.

“Mshitakiwa yuko mbele ya Mahakama hii lakini upelelezi haujakamilika, tunaomba Mahakama itupangie siku nyingine ya kutajwa kutokana na upelelezi kuendelea,” alisema Gavyole.

Kutokana na sababu hizo, Hakimu Haule aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 16 itakapotajwa tena.

Mshitakiwa huyo maarufu kama Scorpion alifikishwa mahakamani hapo akiwa kwenye gari dogo la mizigo tofauti na siku za nyuma ambapo alikuwa akiletwa akiwa kwenye basi la Magereza.

Awali ilidaiwa kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Septemba 9 Buguruni Sheli alipomwibia Mrisho fedha na vitu vyenye thamani ya Sh 476,000 na kumjeruhi kwa kumchoma kisu tumboni, mabegani na machoni.