Wednesday, November 30, 2016

UKIMWI sasa kudhibitiwa

UKIMWI sasa kudhibitiwa kwa njia ya simu

Tanzania imeingia rasmi kwenye mfumo maalum wa kimataifa wa kupata huduma za afya ya UKIMWI kwa njia ya simu bila malipo mfumo ambao umefadhiliwa na nchi ya Marekani.

Akizindua mfumo huo Kaimu Balozi wa Marekani nchini Bi. Virginia Blaser amesema mfumo huo utawafikia zaidi ya watu laki nane huku lengo kuu la mfumo huo likiwa ni kupunguza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi kutoka asilimia 7.5 mpaka asilimia 5 hadi kufikia asilimia 0.0.

Amesema watu wote ambao wanadhaniwa kuwa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi hadi kufikia mwaka 2020 wawe tayari wamepimwa kwa asilimia 90, asilimia 90 waanze kutumia dawa, na asilimia 90 kiwango chao cha maambukizi kiwe kimepungua.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya TAYOA nchini Bw . Peter Masika amesema katika ufadhili wa mfumo huo wao wakiwa ni wasimamizi wa mfumo watahakikisha unawafikia watanzania wote hasa wale wasiofikiwa na huduma muhimu za kiafya na kuwataka watanzania kujitokeza kwa wingi kutumia mfumo huo ili kutokomeza ugonjwa wa Ukimwi.

Chadema: Hatutakubali tena kudhulumiwa 2020

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) ,Vincent Mashinji amesema hawatakubali tena kudhulumiwa kwa namna yoyote  katika uchaguzi wa mwaka 2020.

Dk. Mashinji amesema hayo huku akimtolea mfano wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, na kuongeza kuwa kuna mambo hutokea bila kutarajia lakini watapambana kwa kila hali,

“Huu ni uchaguzi kuna mtu alitarajia haya yaliyofanywa na Jecha? hii inaonyesha kwenye nchi yetu bado kuna tatizo la utendaji haki, wewe umefanya mara ya kwanza tukanyamaza,ukafanya tena mara ya pili kibabe,tukalalamika, badala ya kutuita tuongee, unasema nendeni mkaseme kokote kule”alisema Mashinji.

Aidha, akiongelea utawala wa Rais Magufuli ,Mashinji amesema kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa utawala bora na matokeo yake yeye ndio amekuwa kila kitu, ameongeza kuwa wakati anaanza  mapambano na rushwa aliamini kwamba angeweza kuliondoa tatizo hilo lakini imekuwa tofauti.

Hata hivyo, Mashinji ameongeza kuwa katika mwaka mmoja wa Rais Magufuli, amesema ameshindwa kusimamia utawala bora baada ya kupiga marufuku mikutano ya hadhara pamoja na shughuli zote za kisiasa nchini kwa kile alichosema kuwa muda wa siasa umekwisha.