Mwandishi: SEID BIN SALIM
BORA nikose kibarua kwa ajili yako madam, naomba unisubiri hapo
nje niende nimwambie nimeacha kazi ili japo tuongozane nipajue utapoishi
kwa sasa, tuendeleze udugu wetu sababu umenisaidia mengi sana ambayo
yalinifanya nikuone wewe ni miongoni mwa watu wachache ambao bado wapo
katika dunia hii ya sasa. Nisubiri madam nikaage, kama kazi nitapata
kwengine tu.
“Hapana naomba usifanye hivyo, usiache kazi kwa ajili yangu,
utanipigia simu na nitakuelekeza siku moja utakuja, hii kazi ndiyo
inayoingiza riziki yako usifanye hivyo kabisa,” ni maneno niliyomuambia,
nikamueleza tu aishi naye vizuri hata huyo aliyeingia ili kulinda
kibarua chake.
Nilimuomba anifungulie mlango niondoke, nilitoka na kukodi teksi nikaondoka hadi kwa bibi yako.
Nliishi na bibi yako kipindi chote cha mimba, bado sikukata tamaa
nikijua huenda Mungu atamrudisha nyuma mume wangu akumbuke tulikotoka
lakini wapi, nilikuja kuamini kuwa ndiyo basi tena.
Siku moja nikiwa shambani kwenye hili shamba tunaloishi, maana
alisema ameniachia shamba lote, nilikuwa nalima, ghafla nikaona linapaki
gari kubwa na dogo, lile dogo alikuwemo yeye na huyo mwanamke wake,
kubwa walijaa vijana ambao walishuka akawapa kazi ya kuvuna kila
kilichokuwamo shambani.
sikuweza kuwazuia kwa sababu mwenye mali tayari alikuja, walipomaliza kuvuna akiwa peke yake nilimuuliza.
“Nimekukosea nini lakini mume wangu mpaka unafaya haya yote?” hakujibu
swali langu zaidi ya kunisonya, akaenda alikokuwa mwanamke wake,
wakaingia kwenye gari na kuondoka.
Mimba tayari ilishakuwa kubwa, niliteseka sana, nililazimika kubeba
mzigo wa kuni wakati tumbo tu lilikuwa mzigo tosha kwangu, kiukweli
mpaka najifungua nilipitia mengi sana, nilipojifungua ndipo nikahamia
hapa kwa sababu kwa bibi yako kama unavyopaona kuna chumba kimoja.
Nliumia sana, baba yako alinifanyia visa vingi sana ambavyo hata vingine
havielezeki, naumia, naumia mwanangu nikizingatia nilimuheshimu sana
Masoud lakini…
***
Mama hakuweza kumalizia neno, alianguka kitandani akiwa tayari
amepoteza fahamu, niliumia sana kupata habari nzima ya baba, machozi
wakati wote yalikuwa yakinitoka, nilijikuta nikijuta kuuliza maswali
ambayo yalipelekea mama kupoteza fahamu. Nilianza kuita, “Mama! Mama!,
Mama! Amka!” lakini hakuamka, nilichanganyikiwa nikihisi labda amekufa.
Nilikumbuka darasani kwenye somo la Kiswahili tulifundishwa namna mtu
anavyoweza kuzirai au kuzimia na kupoteza fahamu muda wa nusu saa au saa
nzima, nilijikaza kiume nikachukua mfuniko wa ndoo na kuanza kumpepea
nikiwa nalia huku nikisikilizia ikifika nusu saa bila kuamka niende
kuita majirani waliokuwa mbali kidogo.
Namshukuru Mungu hazikupita dakika kumi mama aliamka, nikamuomba
anisamehe sana kwa kumkumbusha machungu ambayo tayari yalishaanza
kufutika moyoni mwake, niliumia sana kiukweli siku hiyo.
Nilimlaani sana baba yangu japo mama alishaniambia nisimchukie
aliyemfanyia ubaya mtu muhimu katika maisha yangu, lakini nilitengeneza
chuki na kuwachukia wanaume wote wanaowanyanyasa wanawake.
Tokea siku hiyo nikawa nasoma kwa bidii sikuwa na mchezo kwenye
masomo, rafiki asiyehitaji kusoma sikumuhitaji, nilikuwa pamoja na wale
wenye juhudi tu na walimu, nilisoma kwa uchungu ili ikiwezekana siku
moja jina langu liwe miongoni mwa majina makubwa Tanzania nimsaidie
mama’ngu kipenzi alopitia maisha magumu kwa ajili yangu…
***
Hizo zote zilikuwa kumbukumbu za kijana aitwaye Seid akikumbuka stori
aliyopewa na mama yake kuhusu mambo aliyofanyiwa na baba yake.
Kumbukumbu alizozikumbuka akiwa amelala chali kwenye kitanda baada ya
kuwa amefanya shughuli za kutwa nzima.
Zilimfanya amkumbuke sana mama yake aliyekuwa ameenda kulala kwa bibi
usiku huo, macho tayari yalishavimba kwa machozi baada ya kukumbuka
kila kitu alichofanyiwa mama yake huku akijisemea moyoni,
“Mungu nisaidie matokeo yangu ya kidato cha sita yatoke yakiwa mazuri
niingie chuo nije nimsaidie mama. Sijui kwa nini wanaume tunakuwa hivi,
ila yote sawa tu Mungu yu pamoja nawe, umenisomesha kwa tabu nyingi sana
mama yangu, zidi kuniombea nifaulu nikusaidie umeteseka sana!”
Seid alifuta machozi yake yaliyokuwa bado yanaendelea kutoka kutokana
na mambo mazito aliyoyakumbuka yaliyotokea miaka zaidi ya kumi na moja
nyuma, aligeuka akalalia ubavu wa kulia akazima kibatari na kushikwa
usingizi.
Asubuhi na mapema alipoamka alichukua jembe na panga akaingia shambani kwa ajili ya kupalilia baadhi ya mazao na kuchanja kuni.
Tokea azaliwe mpaka anafikisha umri wa miaka 20 hakuwahi kumuona baba
yake na wala hakuhitaji kumuona kwa matendo aliyoyafanya, aliendelea
kuishi na mama yake maisha ya kipekee kuliko kijana yoyote, alimpenda
mama yake kuliko chochote na kumtii kwa kila kitu alichoambiwa akiamini
huyo ndiyo Mungu wake wa duniani.
Mwili wa kijana huyu ulikuwa umetanuka mfano wa miraba sita kutokana
na kazi nzito alizokuwa akizifanya kuingiza japo pesa ndogo ya kupata
hata mboga na chakula kingine, maisha ya tabu yote kijana huyu
aliyapitia, kuna muda alihisi Mungu hawaoni yeye na mama yake ndiyo
maana wanateseka. Alijiuliza kwa nini wengine wanajenga majumba ya
kifahari wakati wao hata kibanda cha udongo hawana.
Ilipofika mida ya saa tatu Bi Najma alirudi toka kwa mama yake na
kumkuta kijana wake shambani, alimuita. Seid aligeuka akamuitikia na
kumsalimia.
“Shikamoo mama!”
“Marahaba mwanangu pole!”
“Nishapoa mama hawajambo huko?
“Ndiyo mwanangu hawajambo.”
“Vipi umenisalimia kwa bibi?”
“Ndiyo na yeye anakusalimia.”
“Haya sawa, mi nipo, namshukuru Mungu umerudi mamaangu, kwa sababu, dah
usiku nimekuwaza sana, hivi ule unga jana uliisha?” alisema akiulizia
chakula nyumbani.
“Hapana ulibaki kidogo tu, usijali lakini kuna mchele nimekuja nao kutoka kwa bibi yako shambani.”
“Wao, leo kumbe wali? Hadi raha ukisikia mtoto hatumwi dukani mamaangu ni hapo.”
“Mhh, hujaacha tu mwanangu?” alisema mama yake huku akiinama na kudokoa vigugu vilivyokuwa vimebakia sehemu aliyolima mwanaye.
“Mtoto hakui kwa mama wee, hapo mboga tu ndo tatizo sasa maisha haya!” aliongea akisimama kumuangalia mama yake.
” Ah! hata tukila hivihivi sawa tu mwanangu ndo maisha yetu tutafanyaje?
Ukishakuwa masikini unatakiwa ukubaliane na kila kitu, ebu lete jembe
nikusaidie upumzike kwanza.”
” Acha tu mama hii ni kazi yangu kama kijana kumsaidia mama,” alisema
akaangalia mfukoni kama kuna chochote, akabahatika kukuta shilingi mia
tano.
“Nina mia tano hapa, bora tununue dagaa fungu la mia tano tuchemshe tutowelee kuliko kula hivihivi.
“Sawa si mbaya pia,” alisema Najma.
Kabla ya kuendelea kupalilia, simu yake Seid iliyokuwa mfukoni
ilianza kuita, alishtuka akapapasa mfuko haraka na kuitoa, kabla ya
kuangalia nani anapiga alitikisa kichwa kisha akamuangalia mama yake
ambaye naye alimuuliza.
“Nini?”
“Ni aibu mamaangu hii, vijana wenzangu wanatumia ma-Samsung
makubwamakubwa, ma-Soft Touch, mimi natumia kisimu hiki cha hali ya
chini, jamaniii!”
“Hebu pokea kwanza simu mwanangu hayo mengine yatafuata.”
Seid aliangalia kwenye skrini akaona jina “Ticha”, alipokea huku mama
akitikisa kichwa na kusema chinichini, “Jamani shida hizi, mpaka mtoto
anajisikia vibaya!”
“Haloo Ticha salam alaykum,” alisema Seid.
“Wassalam, vipi hali bosi wangu?” uliitikia upande wa pili.
“Njema tu Mungu anasaidia.”
“Uko wapi?”
“Niko shambani kwetu huku Kiwengwa.”
“Ok, matokeo yanakaribia kutoka kijana, juzi nlienda wizara ya elimu
nikaona nikuibie vitu. Eee bhana, ndugu yangu umepasua,” alisema wa
upande wa pili.
“Ticha nimepasua nini tena?” aliuliza Seid akiwa anaachia jembe.
“Yaani matokeo yako, yako vizuri vibaya mno, umewaburuza form six, Seid, niamini mimi.”
“Eee!!!
Seid hakuweza kuongea chochote, alikata simu uso wake tayari ukiwa
umepagawa, japo aliambiwa ni ya majibu ya kuibia lakini alijikuta na
furaha sana, machozi yalianza kumleng lenga kumfanya mama yake asogee
karibu na kumuuliza.
“Mwanangu vipi, kuna nini?”
Seid hakuweza kujibu, alimuangalia mama yake kisha akaangalia pembeni,
macho tayari yalishajaa machozi, mama yake alimuuliza tena.
“Nini mwanangu mbona sikuelewi?”
“Mama nimefaulu, nimefaulu mama!! Eti mimi nimefaulu mimi mama…”
aliongea kama mtu asiyejielewa, alikaa chini huku akisema “Asante
Mungu” kwa sauti ya kulia, mama yake alimfuata na kumwambia ni jambo
jema lakini asiamini asilimia mia wakati matokeo hayajatoka, kwa sababu
yeye ni maskini matokeo yanaweza kununuliwa pia anaweza kuwa anataniwa
kwenye simu.
Seid aligeuka na kumuangalia mama yake baada ya kusikia maneno yake.
“Unasemaje mama? Matokeo yangu mimi yanunuliwe? Sina utani na ticha,
ticha ni mtu wangu wa karibu sana lazima alichonambia cha kweli, mama
nshafaulu mimi shida zimeisha, najua naingia chuo mama, naingia tu chuo
mimi, eh asante Mungu.”
“Mwanangu ebu punguza munkari, subiri kwanza hadi yatoke ndo uwe na
furaha ya kufaulu kiasi hicho, usiwe hivyo wewe ni mtu wa chini
mwanangu, mara ngapi matokeo yanachukuliwa na watoto wa wenye mali?”
“Mama Mimi ataenunua matokeo yangu akya-Mungu naapia mbele yako namuua,
nimekulia kwenye maisha ya shida nna dhiki mpaka nazichukia, kitabu mimi
ndo kitaniokoa leo mtu anunue matokeo yangu, nafungua mashtaka au
nampiga kipande mama, vyote vikishindikana mimi napelekwa jela nakuapia
mamaangu, shida nilizonazo hizi watu walete habari za ujinga naua mimi,
naua akya-Mungu!”
Alijikuta anaongea vitu kwa hasira baada ya kuambiwa habari za
ununuaji wa matokeo wakati ameambiwa kabisa na ticha wake kuwa
amewaburuza kidato cha sita.
“Tumuombe Mungu inshallah kwa uwezo wake utapita ila si kujipa uhakika
kiasi hicho, kuna mengi pengine jina lako kalifananisha, usiwe na furaha
ya kiasi hicho mwanangu.”
“Dah, mamaangu kipenzi mbona hivyo? Hakulimiki tena hapa, nimefurahi na
kutibuka pia tuondoke,” aliongea huku machozi ya furaha yakiwa
yanaishiaishia, alinyanyuka akabeba jembe na kumuomba watoke shambani,
alipofika nje ya nyumba yao akatupa jembe chini kisha akamuaga kwenda
kutafuta dagaa.
Baa ya nusu saa alirudi akiwa na dagaa waliokuwa kwenye gazeti,
alimkuta tayari mama yake ameshapika wali, ilibidi amsaidie kupika dagaa
walipomaliza waliweka msosi chini wakala mchana ukapita.
Tokea siku hiyo Seid alikuwa ni kijana wa kuwaza na kuwazua juu ya
matokeo aliyoambiwa na rafiki yake mwalimu wake, kila alivyojiuliza
alishindwa kujijibu huku uso ukiwa na tabasamu kwa kuyafahamu matokeo
yake mapema.
Siku na miezi ilisogea mbele, Seid na mama yake waliendelea kuishi
maisha ambayo Mungu aliwaamulia wakati huo, walipopata chakula walikula
walipokosa walilala njaa, kutokana na nyumba yao kuwa peke yake hakuna
aliyeweza kujua maisha yao yakoje, ilikuwa ni siri yao na Mungu
Miezi sita mbele ilikatika, tarehe 15 siku ambayo ilikuwa ndiyo siku ya
kutoka matokeo ya kidato cha sita ilifika, Seid hakuwa na nauli ya
kwenda mjini siku hiyo ilibidi ampigie rafiki yake anayetumia vifaa vya
Intaneti na kumuomba aangalie majibu kwenye tovuti husika ya NECTA
lakini ilishindikana hakuwa na fedha za kumwezesha kufanya hivyo,
ikabidi afanye juu chini aende mjini akiwa na furaha ya hali ya juu
akiamini moja kwa moja yeye mshindi.
Baada ya kufika alienda hadi sehemu yalipokuwepo makaratasi ya
matokeo, alifika huku akiwambia wenzake aliowakuta, “Kabla sijaangalia
matokeo yangu nimeota kuwa nimeshinda.”
Kimyakimya alifika na kuangalia namba yake kwa kutumia kidole. Ghafla
macho yalimtoka baada ya kuiona, mapigo ya moyo yalianza kwenda mbio
akawa katika hali ya siamini, baadhi ya wenzake walimuuliza.
“Bosi vipi mbona kimya!”
Lilikuwa swali zito sana kwake kulijibu, machozi yalimtiririka kama
baadhi ya wanafunzi ambao walikuta matokeo ya ambayo hawakuyaamini,
wakashindwa kujizuia na kuangua kilio.
Seid hakuweza kuamini alichokiona, maswali mengi yaliingia kichwani
mwake, akawa na msongo wa mawazo, alihisi presha kupanda na kushuka
ghafla, taratibu alianza kuanguka chini na kupoteza fahamu, wenzake
waliokuwa karibu walimdaka wakampeleka chini polepole akiwemo kijana
mmoja aliyekuwa swahiba wake wa karibu aitwae Hamad.
TUKUTANE SEHEMU YA 08